Saturday, 30 August 2014

Mafuta yaliyo bora kwa afya


Mafuta ni muhimu mwilini, isipokuwa yanahitajika kwa kiasi
kidogo; hivyo kuepuka kabisa ulaji wa mafuta huweza kuleta
athari katika mwili, ikiwemo ubongo kutofanya kazi vizuri. Hata hivyo mafuta
yanapotumiwa kwa kiasi kikubwa yanaweza kuleta madhara mwilini. Hivyo ni
muhimu kuwa makini na kiasi cha mafuta kinacholiwa katika kila mlo.
Kuna aina kuu mbili za mafuta; yale yanayopatikana katika vyakula vya asili ya
wanyama na yale yatokanayo na mimea.
i) Mafuta yenye asili ya wanyama
Mafuta yenye asili ya wanyama huwa yameganda katika joto la kawaida.
Mafuta haya ni kama nyama iliyonona, nyama ya nundu, samli, siagi, jibini
na maziwa yenye mafuta. Mafuta haya yana lehemu kwa kiasi kikubwa.
Utumiaji wa mafuta haya huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo,
kuwa na uzito uliozidi na unene uliokithiri au kisukari. Hivyo ni muhimu
kupunguza utumiaji wa mafuta haya.
ii) Mafuta yatokanayo na mimea
Mafuta mengi yatokanayo na mimea huwa katika hali ya kimiminika katika
joto la kawaida na kwa kawaida mafuta haya hayana lehemu. Mafuta haya ni
kama mafuta ya soya, ufuta, karanga, alizeti, mawese, pamba na nazi. Mifano
mingine ni pamoja na mbegu zitoazo mafuta kama za korosho, kweme na
mbegu za maboga. Mafuta haya ndiyo bora zaidi kuyatumia ukilinganisha
na yale yenye asili ya wanyama kwani huboresha afya ya mwili. Hata hivyo ni
muhimu kuyatumia kwa kiasi kidogo.

No comments:

Post a Comment

wasiliana nami