Thursday, 17 July 2014

Nizingatie mambo gani ili kufanikisha ulaji bora?




Vifuatavyo ni vidokezo muhimu vya kukusaidia ili uweze kufanikisha

ulaji bora:

Kula mlo kamili mara tatu kwa siku. Hii hukuwezesha kupata
virutubishi muhimu vinavyohitajika mwilini. Mlo kamili hutokana
na kuchanganya angalau chakula kimoja kutoka katika kila kundi la
vyakula na viliwe kwa kiasi cha kutosha. Makundi hayo ya vyakula
ni :
- Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi. Mfano: vyakula vya nafaka
ni mahindi, ngano, mchele, ulezi, mtama na uwele; mizizi - viazi
vitamu, viazi mviringo, magimbi, viazi vikuu, mihogo; ndizindizi
zote za kupika.
- Vyakula vya jamii ya kunde na vya asili ya
wanyama. Mfano: vyakula vya jamii ya kundemaharagwe,
kunde, njugu mawe, mbaazi, njegere,
choroko, karanga, dengu na fiwi. Vyakula vya asili
ya wanyama- nyama aina zote, samaki, maziwa,
jibini, dagaa, mayai na wadudu wanaoliwa (kama
kumbikumbi, senene na nzige).
- Mbogamboga. Mbogamboga zinajumuisha zile za majani
yanayoliwa (kama majani ya maboga, kunde, matembele,
mchicha, sukuma-wiki, spinachi, kisamvu, mchunga,
figili, mnafu, mlenda), na mbogamboga nyingine kama
karoti, bamia, nyanya, biringanya, maboga, matango,
nyanya chungu na mamung’unya.
- Matunda. Mfano mapera, mabungo, ubuyu, ukwaju,
mananasi, maembe, machungwa, mafenesi, mastafeli,
machenza, zambarau, matopetope, mapesheni, mapapai, mikoche,
maembe ng’ong’o n.k.
- Mafuta na sukari. Mfano: Mafuta; siagi, mafuta ya kupikia mbegu
zitoazo mafuta (kama ufuta, korosho, kweme, karanga n.k) na sukari
(kama sukari nyeupe na sukari guru) .

Kula matunda na mbogamboga kwa wingi kila siku. Mbogamboga
na matunda husaidia kuimarisha mfumo wa kinga mwilini, hivyo
kujikinga na maradhi mbalimbali. Vyakula hivi pia huupatia mwili
makapi-mlo ambayo humfanya mtu ajisikie kushiba na kufanya mtu
ale kwa kiasi, hivyo kupunguza uwezekano wa kuwa na uzito uliozidi
au unene.

Ongeza ulaji wa vyakula vyenye makapi-mlo kwa wingi. Makapimlo
husaidia mfumo wa chakula kufanya kazi kwa ufanisi. Pia
humsaidia mtu kupata haja kubwa kwa urahisi na huchangia katika
kupunguza uwezekano wa kuongezeka uzito, kupata baadhi ya
saratani, magonjwa ya moyo na kisukari. Unaweza kuongeza kiasi
cha makapi-mlo kwa kula matunda na mbogamboga kwa wingi,
nafaka zisizokobolewa kama unga wa dona na ngano (kama atta) na
vyakula vya jamii ya kunde.

Epuka vyakula vyenye mafuta mengi. Mafuta ni muhimu mwilini
lakini yanahitajika kwa kiasi kidogo. Mafuta huongeza uzito kwa
haraka. Ulaji wa mafuta mengi huweza kuleta madhara mwilini kama
vile unene, kuongeza uwezekano wa kupata maradhi sugu kama
magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo kubwa la damu. Unaweza
kupunguza kiasi cha mafuta kwa kubadili njia za mapishi, kama
kuoka, kuchemsha au kuchoma badala ya kukaanga. Pia kuchagua
nyama isiyo na mafuta na kuepuka asusa zenye mafuta mengi.

Epuka kutumia sukari nyingi. Sukari huongeza nishati-lishe mwilini
na hivyo kuchangia ongezeko la uzito wa mwili ambao huweza
kusababisha mtu kupata maradhi sugu yasiyoambukizwa. Matumizi
ya sukari huweza kupunguzwa kwa kunywa vinywaji visivyo na
sukari nyingi, kunywa juisi halisi ya matunda (isiyoongezwa sukari),
kuepuka vyakula vyenye sukari nyingi kama soda, juisi bandia, jamu,
biskuti, keki, chokoleti, kashata na pipi.

Epuka kula vyakula vyenye chumvi nyingi.
Ulaji wa vyakula vyenye chumvi nyingi huongeza
uwezekano wa kupata shinikizo kubwa la damu
na baadhi ya saratani. Matumizi ya chumvi nyingi
huweza kupunguzwa kwa kutumia chumvi kidogo
wakati wa kupika, kuepuka vyakula vyenye chumvi
nyingi au vilivyosindikwa kwa chumvi. Pia jenga
tabia ya kutoongeza chumvi kwenye chakula wakati
wa kula.

Kunywa maji safi, salama na ya kutosha
Kunywa maji angalau glasi nane (lita moja na nusu) kwa siku. Maji
ni muhimu sana mwilini kwani hurekebisha joto la mwili, husaidia
katika uyeyushwaji wa chakula, husafirisha virutubishi kwenda
kwenye seli na huondoa mabaki au uchafu mwilini kwa njia ya jasho,
mkojo n.k. Vilevile maji husaidia kulainisha maungio ya mwili.

Kula asusa zilizobora kilishe. Kuwa mwerevu na muelewa kwa
kuchagua asusa zenye virutubishi vingi na muhimu kama matunda,
maziwa, juisi halisi ya matunda, karanga au korosho. Asusa zitumike
kwa kiasi. Epuka asusa zenye mafuta mengi (kama sambusa, soseji
kababu, chipsi), pia zenye sukari nyingi (kama chokoleti, keki,
pipi, kashata) au zenye chumvi nyingi (kama krispi, soseji) kwani
huweza kusababisha ongezeko kubwa la uzito na uwezekano wa
kupata magonjwa sugu yasiyoambukizwa kama kisukari, saratani,
shinikizo kubwa la damu na maradhi ya moyo. Chagua vyakula
vilivyochemshwa, vilivyookwa au kuchomwa kama ndizi, mihogo,
mahindi na viazi.

No comments:

Post a Comment

wasiliana nami