Sunday, 27 July 2014

juice na matunda



Utofauti wa juice na matunda katika mlo

Juisi halisi ya matunda inaweza kuwa sehemu ya matunda
hata hivyo haiwi badala ya matunda au mbogamboga. Katika
vipimo vitano vya mbogamboga na matunda unavyotakiwa
kutumia kwa siku, juisi inahesabika kama kipimo kimoja tu hata kama umekunywa nyingi kiasi gani. Ina maana kuwa ni lazima pia kula matunda na mbogamboga kila siku kwani yana makapimlo ambayo hayapatikani kwenye juisi. Matunda mengine huliwa na maganda yake ambayo huongeza ubora wake. Kwa maana hiyo, juisi glasi moja kwa siku inatosha ila ukipenda unaweza kunywa zaidi.



Utofauti kati ya juice halisi na juice bandia



Juisi halisi ya matunda ni juisi ambayo inatokana
na kukamuliwa matunda, mara nyingi bila kuongeza maji
au sukari, japo yako aina ya matunda ambayo inakuwa
bora ukiongeza maji kidogo kama vile pesheni, maembe,
mananasi n.k. Juisi halisi za matunda zilizotengenezwa
kiwandani huandikwa “100% juice”, na mara nyingi huwa
na bei ya juu.Juisi bandia ni pamoja na vinywaji vyenye rangi mbalimbali vinavyouzwa madukani, ambavyo ni mchanganyiko wa maji, sukari, rangi na ladha bandia ya matunda. Vinywaji hivi hata kisheria haviruhusiwi kuitwa juisi. Vinapokuwa ndani ya paketi au chupa kwenye lebo huongezewa neno “Drink” na hivyo
kusomeka “Juice-Drink”. Hii ina maana sio juisi halisi ya matunda. Nyingine
zimewekwa juisi kwa kiasi kidogo tu kwa hiyo ukisoma lebo utaona asilimia ya
juisi iliyowekwa.Vinywaji hivi bandia kwa kiasi kikubwa huchangia kuupa mwili nishati-lishe
nyingi na havina virutubishi vingine, hivyo kuchangia ongezeko la uzito; pia huhusishwa na kuongezeka uwezekano wa kupata saratani za aina mbalimbali.Sio kweli kwamba vinywaji hivi vinapokuwa na rangi ya zambarau au nyekundu huongeza damu, bali vinywaji hivyo vimeongezwa rangi ambayo haina virutubishi vyovyote.

Tuesday, 22 July 2014

Matumizi sahihi ya mbogamboga na matunda?



Ni muhimu kula mbogamboga na matunda kwa wingi kila siku, na hasa wakati wa mlo. Unashauriwa kula mbogamboga na matunda ya rangi mbalimbali kwani rangi zinapokuwa za aina mbalimbali ubora huongezeka.Inashauriwa kutumia angalau vipimo vitano vya mbogamboga na matunda kila siku. Mfano wa kipimo kimoja ni kama ifuatavyo:
• Karoti zilizokatwakatwa na kupikwa - kiasi cha ujazo wa
kikombe kimoja cha chai (250mls);
• Mboga za majani zilizopikwa kama mchicha au matembelekiasi
cha ujazo wa kikombe kimoja cha chai (250mls);
• Mboga zisizopikwa (kachumbari/ saladi) - bakuli moja
kubwa ujazo unaoweza kuchukua mlo wa mtu mmoja;
• Chungwa moja;
• Ndizi mbivu kubwa kiasi - moja;
• Tikiti- maji kipande kikubwa kimoja
• Parachichi moja dogo;
• Mapera mawili;
• Juisi glasi moja (250mls)
Mfano: Kwa siku moja (asubuhi hadi usiku) unaweza kula kama ifuatavyo, na
isambazwe katika siku nzima: glasi moja juisi, mapera mawili, mchicha uliopikwa
kiasi cha ujazo wa kikombe kimoja cha chai (250mls), matembele yaliyopikwa
kiasi cha ujazo wa kikombe kimoja cha chai (250mls) saladi bakuli moja.