Lishe

Mtindo bora wa maisha ni upi?


1.
Mtindo bora wa maisha ni ule unaozingatia ulaji bora, kufanya mazoezi
 ya mwili, kuepuka matumizi ya sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku;
kuepuka matumizi ya pombe na kuepuka msongo wa mawazo. Mtindo bora
wa maisha ni muhimu katika kuendeleza na kudumisha afya ya mtu na kuzuia
maradhi, hususan magonjwa sugu yasiyoambukizwa.
Lishe na ulaji bora

2.Je, kuwa na hali nzuri ya lishe kunanipa faida gani?
Unapokuwa na hali nzuri ya lishe ina maana kuwa chakula unachokula
kimeupatia mwili wako nishati-lishe na virutubishi vyote muhimu
ambavyo vinahitajika ili uweze kufanya kazi zake kwa ufanisi. Hii ni pamoja
na ukuaji, ukarabati wa seli zilizoharibika au kuzeeka na kuimarisha mfumo
wa kinga, ambao kazi yake ni kuzuia na kukabiliana na maradhi. Hali nzuri ya
lishe pia huimarisha mfumo wa akili ikiwa ni pamoja na uwezo wa kufikiri na
kukumbuka. Kwa mfano, watoto wanapokuwa na hali nzuri ya lishe ufanisi wao
katika masomo huwa mzuri.

3.Ulaji bora ni nini?
Ulaji bora hutokana na kula chakula chenye mchanganyiko wa angalau
chakula kimoja kutoka katika makundi matano ya vyakula. Chakula hicho
kinatakiwa kiwe cha kutosha kukidhi mahitaji ya mwili. Ulaji bora unatakiwa
kuzingatia mahitaji ya mwili kutokana na jinsi, umri, mzunguko wa maisha
(mfano; utoto, ujana, uzee), hali ya kifiziolojia (mfano;ujauzito, kunyonyesha),
kazi au shughuli na hali ya afya. Ulaji bora huchangia katika kudumisha uzito
wa mwili unaotakiwa na kupunguza maradhi, yakiwemo magonjwa sugu
yasiyoambukizwa.


Mayai yana protini kwa wingi, pia vitamini na madini. Hata hivyo
mayai yana lehemu kwa wingi. Yai moja lina kiasi cha miligramu
213 ya lehemu, ambacho ni kiasi cha lehemu kinachohitajika mwilini kwa siku.
Hivyo ni bora kupunguza matumizi ya mayai, yasizidi matatu kwa wiki na
litumike yai moja tu kwa siku tofauti. Kumbuka vyakula vingine pia vina lehemu
na vilevile mwili hutengeneza lehemu.

Maziwa freshi au mtindi yana virutubishi muhimu hasa protini,
madini na vitamini. Unaweza kutumia maziwa aina yoyote kutegemea matumizi
yake. Hata hivyo maziwa ya mtindi huyeyushwa kwa urahisi zaidi tumboni na pia
husaidia uyeyushwaji wa vyakula vingine na ufyonzwaji wa baadhi ya virutubishi.
Hivyo, maziwa ya mtindi yanapendekezwa zaidi hasa kwa wagonjwa kwani
yanamsaidia mgonjwa kupata virutubishi vingi zaidi kwa haraka. Maziwa ya
mtindi pia yana aina ya bakteria wazuri ambao huweza kuzuia au kutibu fangasi
katika mfumo wa chakula.

Mafuta ni muhimu mwilini, isipokuwa yanahitajika kwa kiasi
kidogo; hivyo kuepuka kabisa ulaji wa mafuta huweza kuleta
athari katika mwili, ikiwemo ubongo kutofanya kazi vizuri. Hata hivyo mafuta
yanapotumiwa kwa kiasi kikubwa yanaweza kuleta madhara mwilini. Hivyo ni
muhimu kuwa makini na kiasi cha mafuta kinacholiwa katika kila mlo.
Kuna aina kuu mbili za mafuta; yale yanayopatikana katika vyakula vya asili ya
wanyama na yale yatokanayo na mimea.

i) Mafuta yenye asili ya wanyama
Mafuta yenye asili ya wanyama huwa yameganda katika joto la kawaida.
Mafuta haya ni kama nyama iliyonona, nyama ya nundu, samli, siagi, jibini
na maziwa yenye mafuta. Mafuta haya yana lehemu kwa kiasi kikubwa.
Utumiaji wa mafuta haya huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo,
kuwa na uzito uliozidi na unene uliokithiri au kisukari. Hivyo ni muhimu
kupunguza utumiaji wa mafuta haya.

ii) Mafuta yatokanayo na mimea
Mafuta mengi yatokanayo na mimea huwa katika hali ya kimiminika katika
joto la kawaida na kwa kawaida mafuta haya hayana lehemu. Mafuta haya ni
kama mafuta ya soya, ufuta, karanga, alizeti, mawese, pamba na nazi. Mifano
mingine ni pamoja na mbegu zitoazo mafuta kama za korosho, kweme na
mbegu za maboga. Mafuta haya ndiyo bora zaidi kuyatumia ukilinganisha
na yale yenye asili ya wanyama kwani huboresha afya ya mwili. Hata hivyo ni
muhimu kuyatumia kwa kiasi kidogo.

1 comment:

wasiliana nami