Sunday, 20 July 2014

Asusa/Snacks bora kwa afya



Asusa ni kiasi kidogo cha chakula ambacho sio mlo kamili, kinachoweza kuliwa bila ya matayarisho makubwa. Mara nyingi huliwa kati ya mlo mmoja na mwingine. Kwa watu wengi hasa wafanyakazi na watoto wa shule ni vigumu kupata milo yote nyumbani na hivyo inabidi wabebe au wanunue kiasi
kidogo cha chakula hasa cha asubuhi na mchana. Mara nyingi aina ya vyakula vinavyopatikana sehemu nyingi ni asusa. Kwa bahati mbaya asusa ambazo zinapatikana kwa urahisi katika sehemu za biashara ni zile zenye mafuta mengi, sukari nyingi au chumvi nyingi ambazo kiafya sio nzuri. Vilevile, mara nyingi mtu anapokuwa na njaa anakuwa na hamu ya kula chakula chochote bila kuchagua. Hivyo unashauriwa yafuatayo:
 
Chagua asusa zenye virutubishi muhimu
Kuwa mwerevu kwa kuchagua asusa zenye virutubishi
muhimu kama matunda, maziwa, juisi halisi ya matunda,
karanga, vyakula vilivyochemshwa au kuchomwa kama
ndizi, magimbi, viazi vikuu, mihogo, mahindi au viazi
vitamu.

Epuka asusa zifuatazo:


- Zilizokaangwa au kupikwa kwa mafuta mengi kama sambusa,
chipsi, vitumbua, mihogo, ndizi na kachori.
- Zenye sukari nyingi kama biskuti, visheti, kashata, keki, chokoleti,
juisi bandia, barafu na soda.
- Zenye chumvi nyingi kama krisps, bisi zenye chumvi nyingi,
soseji nk.
Asusa hizi huweza kuchangia kuongezeka uzito wa mwili na uwezekano wa kupata kisukari, shinikizo kubwa la damu, baadhi ya saratani na magonjwa ya moyo.

No comments:

Post a Comment

wasiliana nami