Sunday, 17 August 2014

Ebola haijaingia nchini - Waziri

Wagonjwa waliohisiwa wamepimwa hawajaambukizwa
.
Wakati hofu ya kuingia kwa ugonjwa wa Ebola nchini ikiwa imetanda, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema hadi sasa hakuna wagonjwa waliobainika kuwa nao.

Juzi wagonjwa wawili, mmoja akiwa raia wa Benin walitiliwa shaka kuwa  na ugonjwa huo, lakini baada  ya vipimo walibainika kuwa na magonjwa ya kawaida.


Raia wa Benin ambaye ni mwanafunzi wa shule moja ya kimataifa hapa nchini, alibainika kuwa na malaria wakati Mtanzania alikuwa na maradhi yake ya muda mrefu. Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,  Nsachris Mwamwaja jana aliwatoa hofu Watanzania kuwa hakuna wagonjwa wa ebola nchini na kueleza kuwa, watu hao waliofikishwa juzi kwenye kituo maalum Temeke wamebainika hawana ugonjwa huo.

Mwamwaja alisema kuwa Mtanzania huyo mfanyabiashara alikuwa akisafiri kwa ndege kutoa Dar es Salaam kuelekea Mbeya, wakati akiwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere, alizidiwa na damu zilianza kumtoka kwenye fizi lakini vipimo vya awali vilionyesha ana maradhi ya muda mrefu (bila kuyataja).

Aidha, alisema mwanafunzi huyo raia wa Benin anayeishi nchini na wazazi wake alikuwa anarejea nchini baada ya kuwa likizo nchini kwao.

“Mwanafunzi huyu juzi alionekana kuwa na dalili ya homa kali, kuumwa kichwa na mwili kuchoka hivyo baada ya kupelekwa hospitali ya AMI na kubainika alitoka nje ya nchi hivi karibuni, uongozi wa hospitali hiyo ulitupigia simu ili tukamchukue kwa ajili ya vipimo vya ugonjwa wa ebola,” alisema na kuongeza:

“Kikosi kazi cha wataalamu waliopewa mafunzo kuhusiana na ugonjwa huo kilifika hapo kumchukua  na kumpeleka Temeke kwenye moja ya eneo lililotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa ebola,” alisema.

Alisema baada ya vipimo alionekana na ugonjwa wa malaria na sio Ebola kama ilivyohisiwa awali.

“Benin hakuna ebola, na katika kujiridhisha tumebaini familia ya mtoto huyu iliyopo nchini humo, haijawahi kutoka nje ya nchi hiyo, pia huyu Mtanzania historia inaonyesha  mara ya mwisho alikuwa Nairobi nchini Kenya,” alisema.

Alisema katika kukabiliana na ugonjwa huo nchini, serikali inaendelea kutoa mafunzo kwa madaktari, wauguzi, wataalum wa maabara na kwa makundi mengine ili itakapotokea nchi kupata mgonjwa iweze kumudumia kitaalam zaidi.

Kuhusu udhibiti kwenye mipaka, alisema wamejitahidi kuhakikisha wataalam hao wanakuwapo wakati wote ili watu wanaoingia nchini wasiwe na virusi vya ugonjwa huo.

Mwamwaja alitaja changamoto kwenye mipaka hiyo kuwa ni maeneo mengi kuwa wazi. “Tunajitahidi kwa upande wa anga, viwanja vya ndege kuna madawati ambayo wapo wataalam waliopata mafunzo ambapo inapotokea mtu akahisiwa uhudumiwa na zipo fomu maalum ambazo mtu anazijaza ambazo taarifa zake ndizo hutusaidia sisi,” alisema.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Seleman Rashid, akizungumza katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jana, alisema watu hao waliolazwa walitiliwa shaka kwamba huenda wana Ebola, hata hivyo baada ya kupimwa ikabainika hawajaambukizwa, lakini bado wako chini ya uangalizi wa madaktari waliopewa mafunzo maalum kukabili ugonjwa huo.

“Tuna wagonjwa ambao tumewalaza lakini kwa mujibu wa dalili walizokuwa nazo hawamo katika wale wagonjwa wenye Ebola,”alisema.
Dk. Rashid alisema serikali imejipanga kukabiliana na ugonjwa huo iwapo utajitokeza nchini na kila mtu anayetiliwa shaka ni lazima achunguzwe kwa kupimwa kama ana ebola au la.

Alisema kimsingi hadi sasa hakuna mtu yeyote mwenye ebola ambaye amegundulika nchini na kwamba waliotiliwa shaka na kupelekwa katika kituo hicho maalum mmoja ni binti ambaye alikuwa ametoka nchini Benin.

Benin ni moja ya nchi za Afrika Magharibi ambako ugonjwa huo umeua watu wengi. Imepakana na Nigeria kwa upande wa mashariki ambayo kuna uthibitisho wa vifo vinne. Vifo vingine vimeripotiwa Liberia 282, Guinea 363 na Sierra Leone 286.

Juzi Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Grace Maghembe, alipopigiwa simu na NIPASHE kuulizwa juu ya taarifa za kuwapo kwa wagonjwa wa Ebola jijini Dar es Salaam, alisema muda huo alikuwa ‘bize’ kuwashughulikia watu waliohisiwa kuwa na Ebola na kuomba apigiwe simu baada ya saa moja.

EBOLA NI NINI
Ugonjwa wa Ebola unaenea kwa kasi kwa kuambukizwa na kirusi kinachopatikana katika ukanda wa nchi za joto. Dalili za ugonjwa huo ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa na vidonda kooni.

Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanyakazi na kwa baadhi ya wagonjwa kutoka damu ndani na nje ya mwili.

Hadi sasa watu 1,069 wamekufa kwa ugonjwa huo wengi wakiwa ni barani Afrika na mmoja aliyefia Uhispania.

SHIRIKA LA AFYA DUNIANI (WHO)
Who juzi ilitahadharisha kuwa Kenya inaweza kuwa katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa huo kutokana na kasi ya kuenea kwake Barani Afrika.

Hofu hiyo inaelezwa kutokana na Kenya kuwa kitovu cha usafiri wa ndege kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati huku wasafiri wengi wanaokwenda na kurudi kutoka nchi za Afrika Magharibi wakipitia jijini Nairobi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

wasiliana nami