Sunday, 20 July 2014

Uhusiano uliopo kati ya afya ya mtoto na ulaji wake




Tafiti zimeonesha kuwa kuna uhusiano kati ya ulishaji wa mtoto na
uwezekano wa kupata magonjwa sugu yasiyoambukizwa utotoni, katika ujana na hata anapokuwa mtu mzima.Tafiti hizo zimeonyesha kuwa:

• Unyonyeshaji wa maziwa ya mama huwakinga watoto dhidi ya kuwa na
uzito uliozidi na unene uliokithiri wanapokuwa wadogo na hapo baadae.

• Watoto walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa muda mfupi (chini ya miezi sita) na wale waliopewa maziwa mbadala (maziwa ya kopo au ya wanyama) wako katika hatari zaidi ya kupata baadhi ya magonjwa sugu yasiyoambukizwa kama kisukari, shinikizo kubwa la damu na saratani utotoni, katika ujana na wanapokuwa watu wazima.

• Ulishaji wa vyakula vya nyongeza vyenye nishati-lishe kwa wingi
unahusishwa na mtoto kuwa na hatari ya
kupata unene, saratani na shinikizo kubwa la
damu ukubwani.

• Unene wakati wa utoto humuweka mtoto katika hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyoambukizwa kama kisukari na ugonjwa wa moyo.Hivyo, mtoto akinyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo na baada ya miezi sita kupewa chakula cha nyongeza kama inavyoshauriwa huku mtoto akiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama mpaka anapotimiza umri wa miaka miwili au zaidi; kunachangia katika kumkinga mtoto huyu dhidi ya magonjwa sugu yasiyoambukizwa pamoja na utapiamlo ambao pia huweza kuleta madhara mengine utotoni na katika utu uzima. Vilevile, mama anaponyonyesha humpunguzia uwezekano wa kupata saratani ya matiti.





Asusa/Snacks bora kwa afya



Asusa ni kiasi kidogo cha chakula ambacho sio mlo kamili, kinachoweza kuliwa bila ya matayarisho makubwa. Mara nyingi huliwa kati ya mlo mmoja na mwingine. Kwa watu wengi hasa wafanyakazi na watoto wa shule ni vigumu kupata milo yote nyumbani na hivyo inabidi wabebe au wanunue kiasi
kidogo cha chakula hasa cha asubuhi na mchana. Mara nyingi aina ya vyakula vinavyopatikana sehemu nyingi ni asusa. Kwa bahati mbaya asusa ambazo zinapatikana kwa urahisi katika sehemu za biashara ni zile zenye mafuta mengi, sukari nyingi au chumvi nyingi ambazo kiafya sio nzuri. Vilevile, mara nyingi mtu anapokuwa na njaa anakuwa na hamu ya kula chakula chochote bila kuchagua. Hivyo unashauriwa yafuatayo:
 
Chagua asusa zenye virutubishi muhimu
Kuwa mwerevu kwa kuchagua asusa zenye virutubishi
muhimu kama matunda, maziwa, juisi halisi ya matunda,
karanga, vyakula vilivyochemshwa au kuchomwa kama
ndizi, magimbi, viazi vikuu, mihogo, mahindi au viazi
vitamu.

Epuka asusa zifuatazo:


- Zilizokaangwa au kupikwa kwa mafuta mengi kama sambusa,
chipsi, vitumbua, mihogo, ndizi na kachori.
- Zenye sukari nyingi kama biskuti, visheti, kashata, keki, chokoleti,
juisi bandia, barafu na soda.
- Zenye chumvi nyingi kama krisps, bisi zenye chumvi nyingi,
soseji nk.
Asusa hizi huweza kuchangia kuongezeka uzito wa mwili na uwezekano wa kupata kisukari, shinikizo kubwa la damu, baadhi ya saratani na magonjwa ya moyo.